Wednesday, February 16, 2011

Mabomu yalipuka Kambi ya Jeshi Gongo la mboto

Mabomu yamelipuka mfululizo Jumatano usiku katika kambi ya jeshi la Tanzania, Gongo la Mboto, kilomita chache kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. Hakuna ripoti rasmi kutoka serikali ya Tanzania wala madhara yaliyotokana na milipuko hiyo.

Kulingana na wakazi wa karibu na eneo la Gongo la Mboto milipuko hiyo ilianza kiasi cha saa mbili na dakika 35 Jumatano usiku na ilikuwa inaendelea mfululizo hadi karibu saa tano usiku. Wakazi wengi wa maeneo ya jirani wamekimbia nyumba zao kujiepusha na athari za milipuko hiyo.

Milipuko kama hiyo ilitokea katika kambi ya jeshi ya Mbagala mjini Dar es Salaam Aprili 9, 2009 ambapo watu 26 walikufa na wengine 636 kujeruhiwa. Watu zaidi ya elfu tisa walipoteza makazi yao katika milipuko ya Mbagala.

Wakazi wa eneo karibu na Gongo la Mboto wanasema huenda milipuko hii ni mikubwa kuliko ile ya Mbagala.

No comments:

Post a Comment